Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza Mpaka la Sita I – VI

Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza Mpaka la Sita I – VI

Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza mpaka la Sita I – VI ni mfumo rasmi wa masomo unaotumika kuwajenga wanafunzi kielimu na kimaadili katika hatua za awali za elimu nchini Tanzania. Mtaala huu unazingatia maendeleo ya jumla ya mwanafunzi, ukilenga kumwezesha kupata maarifa, ujuzi, na maadili yanayohitajika kwa maisha ya kila siku na maendeleo ya kitaaluma. Kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, mtaala huu unahakikisha kuwa mwanafunzi anapitia masomo muhimu kama Kiswahili, Hisabati, Sayansi, na maarifa mengine ya kijamii, huku pia ukitilia mkazo uzalendo na maadili ya Kitanzania.

Mtaala mpya ulioboreshwa wa Elimu ya Msingi Darasa I – VI umeandaliwa kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023, maoni ya wadau yaliyokusanywa na kuchakatwa kati ya mwaka 2021 na 2022 na matokeo ya uchambuzi wa maandiko kuhusu uzoefu kutoka nchi nyingine. Mtaala huu unazingatia dira ya elimu inayolenga kumwandaa Mtanzania aliyeelimika, na mwenye maarifa, stadi na mitazamo chanya anayethamini usawa, haki na elimu bila ukomo katika kuleta maendeleo endelevu ya kitaifa na kimataifa.

Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza Mpaka la Sita I – VI

Vilevile, Mtaala huu umezingatia malengo makuu ya elimu pamoja na malengo ya elimu ya msingi nchini Tanzania. Kwa kuzingatia haya, Mtaala huu umeweka viwango vya utoaji wa elimu katika ngazi ya Elimu ya Msingi kwa kubainisha ujuzi, maarifa, stadi na mwelekeo atakaoujenga mwanafunzi, umahiri wa jumla, maeneo makuu ya ujifunzaji, umahiri mkuu na mahususi, njia za ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Mtaala umebainisha muda utakaotumika katika utekelezaji, lugha ya kujifunzia na kufundishia, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na njia zitakazotumika kupima maendeleo ya mwanafunzi kwa kuzingatia ujenzi wa umahiri. Hali kadhalika, Mtaala umebainisha sifa za kitaaluma na kitaalamu za mwalimu ambaye ndiye mtekelezaji mkuu wa Mtaala katika ngazi ya shule.

Pamoja na matamko mbalimbali ya kisera na miongozo ya kitaifa, kikanda na kimataifa, Mtaala huu umezingatia nadharia za ukuaji na ujifunzaji na Falsafa ya Elimu ya Kujitegemea inayosisitiza utoaji wa elimu inayomwezesha Mtanzania kujitegemea na kumudu maisha yake ya kila siku. Hivyo, utekelezaji wake utawezesha ukuaji wa mwanafunzi kimwili, kiakili, kihisia na kijamii. Ni matarajio yangu kuwa kupitia Mtaala huu, mwalimu atamwezesha mwanafunzi kujenga umahiri uliokusudiwa. Aidha, wasimamizi wote wa utekelezaji wa Mtaala na wadau wengine wa Elimu ya Msingi nchini watahakikisha kuwa elimu inayotolewa inakidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa, kikanda na kimataifa.

CLICK HERE TO DOWNLOAD PDF